1 Samuel 16:1-13

Samweli Anamtia Daudi Mafuta

1 a Bwana akamwambia Samweli, “Utamlilia Sauli mpaka lini, maadamu nimemkataa asiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli? Jaza pembe yako mafuta, ushike njia uende; ninakutuma kwa Yese huko Bethlehemu. Nimemchagua mmoja wa wanawe kuwa mfalme.”

2 bLakini Samweli akasema, “Nitakwendaje? Sauli atasikia juu ya jambo hili na ataniua.”

Bwana akamwambia, “Chukua mtamba wa ngʼombe na useme, ‘Nimekuja kumtolea Bwana dhabihu.’
3 cMwalike Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakalofanya. Utamtia mafuta kwa ajili yangu yule nitakayekuonyesha.”

4 dSamweli akafanya kile Bwana alichosema. Alipofika Bethlehemu, wazee wa mji wakatetemeka walipomlaki. Wakauliza, “Je, umekuja kwa amani?”

5 eSamweli akajibu, “Ndiyo, kwa amani; nimekuja kumtolea Bwana dhabihu. Jiwekeni wakfu na mje kwenye dhabihu pamoja nami.” Ndipo akamweka Yese wakfu pamoja na wanawe na kuwaalika kwenye dhabihu.

6 fWalipofika, Samweli akamwona Eliabu, naye akafikiri, “Hakika mpakwa mafuta wa Bwana anasimama hapa mbele za Bwana.”

7 gLakini Bwana akamwambia Samweli, “Usitazame sura yake wala kimo chake, kwa kuwa nimemkataa. Bwana hatazami katika vile vitu mwanadamu avitazamavyo. Mwanadamu hutazama katika sura ya nje, lakini Bwana hutazama moyoni.”

8 hKisha Yese akamwita Abinadabu na kumpitisha mbele ya Samweli. Lakini Samweli akasema, “Hata huyu Bwana hakumchagua.” 9 iKisha Yese akampitisha Shama, lakini Samweli akasema, “Wala huyu Bwana hakumchagua.” 10Yese alikuwa na wana saba aliowapitisha mbele ya Samweli, lakini Samweli akamwambia, “Bwana hajawachagua hawa.” 11 jHivyo akamuuliza Yese, “Je, hawa ndio wana pekee ulio nao?”

Yese akajibu, “Bado yuko mdogo kuliko wote, lakini anachunga kondoo.”

Samweli akasema, “Tuma aitwe; hatutaketi mpaka afike.”

12 kBasi akatuma aitwe naye akaletwa. Alikuwa mwekundu, mwenye sura nzuri na umbo la kupendeza.

Ndipo Bwana akasema, “Inuka na umtie mafuta, huyu ndiye.”

13 lBasi Samweli akachukua ile pembe ya mafuta na kumtia mafuta mbele ya ndugu zake, kuanzia siku ile na kuendelea Roho wa Bwana akaja juu ya Daudi kwa nguvu. Kisha Samweli akaenda zake Rama.

Copyright information for SwhNEN